Sunday, 10 August 2014

SHINIKIZO LA DAMU

Vipi kuhusu shinikizo la damu yako? Je, maisha
yako ya sasa yaweza kupandisha shinikizo la damu
katika siku zijazo? Unaweza kufanya nini ili kudhibiti
shinikizo la damu yako? *
Shinikizo la damu ni msukumo wa damu kwenye
kuta za mishipa. Shinikizo la damu laweza kupimwa
kwa ukanda wa mpira unaoweza kujazwa hewa.
Ukanda huo hufungwa kwenye sehemu ya juu ya
mkono na kuunganishwa na kifaa cha kurekodi
shinikizo. Kifaa hicho hurekodi vipimo viwili. Kwa
mfano, chaweza kurekodi kipimo cha 120/80. Nambari
ya kwanza huonyesha kipimo cha shinikizo la damu
wakati moyo unapopiga ( systole). Nambari ya pili
huonyesha kipimo cha shinikizo la damu katikati ya
mapigo ya moyo (diastole ). Shinikizo la damu
hupimwa kulingana na milimeta za zebaki. Madaktari
husema kwamba shinikizo la damu ya mgonjwa
limepanda wakati kipimo kinapozidi 140/90.
Nini hupandisha shinikizo la damu? Hebu wazia
unamwagilia shamba lako maji. Unapofungua mfereji
au unapopunguza ukubwa wa shimo la mfereji,
unaongeza shinikizo la maji. Ndivyo ilivyo pia na
shinikizo la damu. Shinikizo la damu hupanda wakati
damu nyingi inapopita mshipani au wakati mshipa
unapokuwa mwembamba. Mtu hupataje ugonjwa huo?
Mambo mengi yanahusika.
Mambo Usiyoweza Kuepuka
Watafiti wamegundua kwamba iwapo mtu ana watu
wa familia wenye tatizo la kupanda kwa shinikizo la
damu, basi anakabili uwezekano mkubwa zaidi wa
kupata ugonjwa huo. Takwimu zinaonyesha kwamba
mapacha wanaofanana hupata ugonjwa huo zaidi ya
mapacha wasiofanana. Uchunguzi mmoja ulizungumza
juu ya “kuchunguza habari zinazopatikana katika
chembe za urithi ambazo husababisha tatizo la
kupanda kwa shinikizo la damu.” Hiyo inathibitisha
kwamba kuna chembe za urithi zinazosababisha tatizo
la kupanda kwa shinikizo la damu. Inasemekana
kwamba uwezekano wa kupata tatizo hilo huongezeka
mtu anapozidi kuzeeka, na kwamba wanaume weusi
wanakabili uwezekano mkubwa zaidi wa kupata
ugonjwa huo.
Mambo Unayoweza Kuepuka
Tilia maanani lishe bora! Shinikizo la damu ya watu
fulani linaweza kupanda wanapokula chumvi
(sodiamu). Hiyo inahusu hasa wagonjwa wa kisukari,
watu ambao shinikizo la damu yao hupanda sana,
wazee, na watu fulani weusi. Mafuta mengi katika
damu yanaweza kufanyiza utando wa kolesteroli
kwenye kuta za ndani za mishipa. Hivyo, mishipa
huwa myembamba na shinikizo la damu huongezeka.
Watu ambao ni wazito kupita kiasi kwa asilimia 30
wanaweza kupata tatizo la kupanda kwa shinikizo la
damu. Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba
kula vyakula vingi vyenye potasiamu na kalisi
kwaweza kupunguza shinikizo la damu.
Uvutaji wa sigara unaweza kusababisha utando
mgumu wa mafuta kwenye kuta za mishipa, ugonjwa
wa kisukari, mshtuko wa moyo, na kiharusi. Kwa hiyo,
mvutaji wa sigara aliye na tatizo la kupanda kwa
shinikizo la damu anaweza kupata magonjwa ya moyo.
Ijapokuwa uthibitisho unapingana, mfadhaiko na
kafeini—inayopatikana katika kahawa, chai, na
vinywaji vya kola—yaweza kusababisha tatizo la
kupanda kwa shinikizo la damu. Kwa kuongezea,
wanasayansi wanajua kwamba kunywa kileo mara
nyingi na kupita kiasi na kutofanya mazoezi kwaweza
kuongeza shinikizo la damu.
Kutunza Afya
Si jambo la busara kungoja hadi upate tatizo la
kupanda kwa shinikizo la damu ndipo uanze kuchukua
hatua zinazofaa. Mtu anapaswa kutunza afya toka
anapokuwa kijana. Kutunza afya sasa kutafanya
maisha yako yawe mazuri wakati ujao.
Mwafikiano wa Tatu wa Brazili Kuhusu Kupanda
kwa Shinikizo la Damu ulionyesha mabadiliko fulani
maishani ambayo yanaweza kupunguza tatizo hilo.
Madokezo hayo yatawasaidia watu wasio na ugonjwa
huo na wale wanaougua ugonjwa huo.
Watafiti walipendekeza kwamba watu walionenepa
kupita kiasi wanapaswa kula lishe kamili isiyo na
kalori nyingi, kufanya mazoezi ya kiasi kwa ukawaida,
na kuepuka mbinu za kupunguza uzito haraka.
Walipendekeza kwamba watu watumie gramu sita tu
za chumvi au kijiko kidogo tu cha chumvi kila siku. *
Hiyo inamaanisha kutumia kiasi kidogo tu cha chumvi
wakati wa kutayarisha mlo, na pia kutokula sana
vyakula vinavyouzwa makoponi, nyama baridi
zilizopikwa (salami, hemu, soseji, na kadhalika), na
vyakula vilivyokaushwa kwa moshi. Mtu anaweza
kupunguza matumizi yake ya chumvi kwa kuepuka
kuongeza chumvi anapokula na kwa kuchunguza
vibandiko vilivyowekwa kwenye makopo ya vyakula
vilivyotengenezwa viwandani ili kuona kiasi cha
chumvi ambacho kimetumiwa.
Vilevile, Mwafikiano wa Brazili ulidokeza kula
vyakula vingi vyenye potasiamu kwa kuwa vinaweza
“kuzuia kupanda kwa shinikizo la damu.” Kwa hiyo,
lishe bora yapaswa kuhusisha “vyakula vilivyo na
chumvi kidogo na potasiamu nyingi,” kama vile
maharagwe, mboga za kijani iliyokoza, ndizi, matikiti,
karoti, viazi-sukari, nyanya, na machungwa. Ni
muhimu pia kutokunywa kileo kupita kiasi. Watafiti
fulani wanasema kwamba wanaume walio na ugonjwa
wa kupanda kwa shinikizo la damu hawapaswi kunywa
zaidi ya mililita 30 za kileo kila siku; wanawake na
vilevile watu ambao si wazito sana hawapaswi kunywa
zaidi ya mililita 15 za kileo. *
Mwafikiano wa Brazili ulikata shauri kwamba
kufanya mazoezi ya mwili kwa ukawaida hupunguza
shinikizo la damu na hupunguza uwezekano wa kupata
ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu. Kuna
faida kufanya mazoezi kwa kiasi kama vile, kutembea,
kuendesha baiskeli, na kuogelea, kwa siku tatu hadi
tano kila juma kwa muda wa dakika 30 hadi 45. *
Mambo mengine yanayochangia afya bora yanatia
ndani kuacha kuvuta sigara, kudhibiti ugonjwa wa
kisukari na kiasi cha mafuta katika damu (kolesteroli
na triglyceride ), kula vyakula vyenye kalisi na magnesi
ya kutosha, na kuepuka uchovu na kufadhaika kupita
kiasi. Dawa fulani zaweza kuongeza shinikizo la
damu, kama vile dawa za kuzibua pua, dawa za
kutuliza kiungulia zilizo na sodiamu nyingi, dawa za
kudhibiti hamu ya kula, na dawa za kumaliza maumivu
ya kichwa na kichefuchefu zilizo na kafeini.
Kwa wazi, iwapo shinikizo la damu yako hupanda,
daktari wako anaweza kukushauri kuhusu lishe na
mazoea yako kulingana na mahitaji yako binafsi. Hata
hivyo, kutunza afya tangu ujanani ni jambo lenye
manufaa kwa watu walio na tatizo la kupanda kwa
shinikizo la damu na kwa washiriki wote wa familia.
Marian, aliyetajwa mwanzoni mwa makala hii,
alilazimika kufanya mabadiliko maishani mwake.
Ijapokuwa yeye ni mgonjwa, sasa anatumia dawa na
anafurahia maisha. Vipi wewe? Endelea kudhibiti
shinikizo la damu yako huku ukisubiri wakati ambapo
watu wote watakuwa na afya bora na “hapana
mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”— Isaya 33:24 .
[Maelezo ya Chini]
Gazeti la Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote
mahususi, kwani huo ni uamuzi wa mtu binafsi.
Iwapo una ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la
damu, ugonjwa wa moyo, wa ini, au wa figo na
unatumia dawa, muulize daktari wako kuhusu
kiasi cha chumvi na potasiamu ambacho unahitaji
kila siku.
Kileo cha mililita 30 kinalingana na mililita 60 za
vinywaji kama wiski, vodka, na kadhalika, mililita
240 za divai, au mililita 720 za pombe.
Zungumza na daktari wako kuhusu mpango wa
kufanya mazoezi.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
KUPAMBANA NA UGONJWA WA KUPANDA KWA
SHINIKIZO LA DAMU
1. Mambo Yanayoweza Kusaidia Kudhibiti Kupanda
kwa Shinikizo la Damu
• Punguza uzito wa mwili
• Punguza kiasi cha chumvi unachotumia
• Kula vyakula vingi vyenye potasiamu
• Usinywe sana vileo
• Fanya mazoezi kwa ukawaida
2. Mambo Mengine Yanayoweza Kusaidia Kudhibiti
Shinikizo la Damu
• Tumia vidonge vyenye kalisi na magnesi
• Kula vyakula vyenye makapi mengi tu
• Dhibiti mfadhaiko
3. Madokezo ya Ziada
• Acha kuvuta sigara
• Dhibiti kiwango cha kolesteroli mwilini
• Dhibiti ugonjwa wa kisukari
• Usitumie dawa zinazoweza kuongeza shinikizo la
damu

No comments:

Post a Comment