Je, Unafanya Mazoezi ya Kutosha?
“Kuwa na ratiba ya kufanya mazoezi kwa ukawaida kunaweza kunufaisha zaidi kuliko dawa yoyote iliyopo au itakayovumbuliwa wakati ujao.”
MANENO hayo yaliandikwa mwaka wa 1982 na Dakt. Walter Bortz wa Pili, profesa wa dawa wa chuo kikuu. Kwa miaka zaidi ya 23 iliyopita, wataalamu na mashirika mengi ya afya yamenukuu maneno hayo katika vitabu, magazeti, na vituo vya Intaneti. Uthibitisho uliopo unaonyesha kwamba ushauri huo uliotolewa na Dakt. Bortz bado unatumika leo sawa na ulivyotumika mwaka wa 1982, na bado unakubaliwa kuwa unafaa na sahihi. Kwa hiyo tunapaswa kujiuliza, ‘Je, ninafanya mazoezi ya kutosha?’
Wengine wamekata kauli kimakosa kwamba hawahitaji kufanya mazoezi kwa sababu wao si wazito kupita kiasi. Watu wanene na wazito kupita kiasi wanaweza kunufaika sana kwa kufanya mazoezi kwa ukawaida, lakini hata ikiwa wewe si mzito kupita kiasi, kufanya mazoezi zaidi kunaweza kuboresha afya yako na kusaidia kuzuia magonjwa hatari kutia ndani aina fulani za kansa. Pia uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mazoezi yanaweza kupunguza wasiwasi na huenda hata yakazuia mshuko wa moyo. Ukweli ni kwamba watu wengi wembamba hupatwa na mfadhaiko wa kiakili na kihisia, magonjwa ya moyo, kisukari, na matatizo mengine ambayo huzidishwa na kutofanya mazoezi ya kutosha. Kwa hiyo, iwe wewe ni mzito kupita kiasi au sivyo, na ikiwa hufanyi mazoezi, unapaswa kufanya mabadiliko.
Mazoezi ya Kutosha Yanahusisha Nini?
Utajuaje ikiwa unafanya mazoezi ya kutosha? Watu wengi wana maoni mbalimbali kuhusu mazoezi ya kutosha. Hata hivyo, wataalamu wengi wa afya wanakubaliana na mambo fulani ya msingi ambayo yanawahusu watu wengi. Mashirika kadhaa ya afya yalieleza kwamba hufanyi mazoezi ya kutosha ikiwa (1) hufanyi mazoezi au kazi fulani ngumu kwa angalau dakika 30 mara tatu kwa juma, (2) unafanya shughuli zako za kujistarehesha ukiwa mahali pamoja, (3) mara nyingi hutembei umbali wa meta 100 hivi kwa siku, (4) unaketi mchana kutwa, (5) unafanya kazi ambayo haihitaji nguvu nyingi.
Je, unafanya mazoezi ya kutosha? Ikiwa hufanyi, anza leo. Lakini huenda ukasema, ‘sina wakati.’ Unapoamka asubuhi wewe huwa umechoka sana. Siku inapoanza, una wakati mchache sana wa kujitayarisha na kufika kazini. Kisha, baada ya siku yenye shughuli nyingi, unajihisi kwamba umechoka sana hivi kwamba huwezi kufanya mazoezi au una mambo mengine mengi ya kufanya.
Au huenda wewe ni miongoni mwa watu ambao huanza kufanya mazoezi lakini huacha baada ya siku chache tu kwa sababu ya kuona yanachosha au kujihisi mgonjwa baada ya kufanya mazoezi. Wengine hawafanyi mazoezi kwa sababu wao hufikiri ratiba nzuri lazima itie ndani mazoezi magumu ya kuinua vyuma, kukimbia kilometa nyingi kila siku, na kufuata mpangilio fulani wa mazoezi ya kunyoosha viungo.
No comments:
Post a Comment