Upangaji wa mlo gani wa kula kwa siku husika ni mojawapo wa mambo yanayosumbua sana kila asubuhi unavyoanza siku maana inabidi uhakikishe familia yako inakula mlo kamili na tofauti tofauti. Ni vyema ukawa na utaratibu wa kupanga ratiba ya mlo kwa wiki nzima na kazi hii unaweza kuifanya ijumaa jioni ukiwa umepumzika. Kufanya hivi kutakusaidia kujua ununue nini kwa wakati huo na itakupunguzia kufikiria kila asubuhi kitu cha kupika na itakuwezesha kula vyakula bora na vilivyoandaliwa kwa umakini.
Kwanza orodhesha vyakula mbalimbali ambavyo huwa mnatumia nyumbani kwako katika makundi ya vitafunwa, chakula kikuu na mboga na kisha anza kupanga kwa siku kutokana na upatikanaji wake kwa wiki husika na vile vile muda wa kuviandaa. Mfano wa vitafunwa ni mikate, chapati, mihogo, maandazi, sausage, kiporo n.k, mifano wa chakula kikuu ni ugali, wali, viazi, ndizi, makande n.k na mfano wa mboga ni nyama, samaki, mchicha, kabichi, kisamvu n.k.
Unapopanga ratiba ya wiki pia unaandaa orodha ya vile uavyohitaji kununua kwa ajili ya wiki husika na ndio maana nikasema ukiipanga ijumaa jioni ni vyema ili jumamosi ufanye manunuzi ambayo yanahitajika na mengine madogo unaweza fanya katikati ya wiki. Ratiba hii uiweke mahali panapoonekana jikoni ili wote mnaohusika na kuandaa chakula mfahamu mapema nini kitaandaliwa siku fulani na nini kinahitajika kufanya.
No comments:
Post a Comment